SERIKALI YAONYA VIONGOZI WA DINI , KUJIHUSISHA KISIASA UVUNJIFU WA AMANI


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo , akihutubia waumini wa dini ya Kiislam ya Jumuiya ya Ahamadia (hawapo pichani)  
Na  Mashaka Baltazar,MWANZA
  SERIKALI imesema migogoro ya kisiasa na kiitikadi ya kidini, kutokuwepo kwa mgawanyo sawa wa rasimali za nchi kunaweza kuleta uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.
  Pia imewaonya wanasiasa na viongozi wa dini wanaochanganya siasa na mambo ya kiroho, kwa kisingizio cha cha dini kuacha kufanya hivyo, kwani wanasababisha uvunjifu wa amani.
  Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo, katika mkutano wa amani uliondaliwa na Jumuiya ya Waislamu ya Ahamadiya jijini hapa, mkutano ambao ulihudhuriwa na Amiri Sheikh Mkuu wa Jumuiya hiyo nchini, Tahir Mahamood , pamoja na viogozi mbalimbali wa madhehebu ya dini ya kiislamu na kikristo jijini .
  Ndikilo alisema, wapo viongozi wa dini wanachanganya siasa na mambo ya kiroho , wanapofanya hivyo wanavuruga amani ya nchi yetu na kuingiza jamii katika machafuko, ambapo aliwataka viongozi hao na wanasiasa kuacha kuchanganya mambo hayo kwani yatasababisha amani ya nchi yetu kuvurugika.
  “Dini ni kumcha Mungu, lakini siasa ni kuchukua dola au madaraka ya nchi.Wapo baadhi ya viongozi wa dini wanachanganya siasa na mambo ya kiroho, hao wanasababisha uvunjifu wa amani.Siasa tuwachie wanasiasa kwenye majukwaa yao.Serikali inawaunga mkono kutokana na juhudi zetu za kulinda na kutunza amani tuliyo nayo,” alisema Ndikilo.

Comments