NHIF YATOA MAFUNZO KWA WATAALAMU WA AFYA KUTOKA ZAMBIA


 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya, Emanuel Humba akizungumza na Ujumbe
kutoka Zambia ambao umefika kwa lengo la kujifunza
namna Mfuko huo unavyofanya kazi.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya, Hamis Mdee akitoa maelezo ya namna NHIF inavyofanya kazi kwa ujumbe huo muda mfupi kabla ya kuanza mafunzo.
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeziomba  nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kubadilishana uzoefu katika kuwahudumia wananchi wao kwenye setka ya afya.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Emanuel Humba wakati akizungumza  na ujumbe kutoka Zambia ambao upo hapa nchini kujifunza kuhusu utendaji wa Mfuko huo.
Bwana Humba amesema nchi za Afrika Mashariki na Kati zina mazingira yanayofanana  na zina changamaoto sawa za utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya, hivyo ni vizuri kubadlishana uzoefu katika kuzikabili.
Amesema ili huduma za afya zitolewe kwa mafanikio ni vema watendaji wa sekta ya Afya  katika  Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wakajenga mazoea ya kukutana na kubadilishana uzoefu mara kwa mara.
Naye Kiongozi wa Ujumbe huo kutoka Zambia, Bwana Mubita Luwabelwa amekiri  kuvutiwa na utendaji na mafanikio ya Mfuko wa Taifa wa Bima y Afya (NHIF) na ndio sababu iliyowafanya wakaja kujifunza kutoka hapa nchini ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi wao kama NHIF inavyofanya hapa nchini.
Bwana Luwabelwa amesema  yeye na ujumbe wake wanaona fahari kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ya ukanda wa Afrika Mashariki badala ya kwenda nchi za magharibi kwa kuwa nchi hizi zina mazingira yanayofanana.
 Ujumbe huo wa watu wanne ambao utakuwa hapa nchini kwa siku nne umewasili hapa nchini Jumapili, unajumuisha maofisa kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini Zambia.
Kwa upande wake Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Judith Kangoma amesema kitendo cha ujumbe wa Wazambia kuja kujifunza ni mwendelezo wa ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi mbili hizo.
“Tunayo mifano mingi ya ushirikiano wetu na Tanzania kama reli ya TAZARA na  bomba la mafuta la TAZAMA hivyo ujumbe huu kuja kujifunza kuhusu uendeshaji wa Mifuko ya Afya ni jambo la msingi kwa kuwa Tanzania imefanikiwa sana katika suala hili,” alisema Balozi.
Alisema anaamini kuwa baada ya ujumbe huu kujifunza na kupata uzoefu kutoka NHIF, watatumia uzoefu huo katika kuendeleza shughuli za uendeshaji wa Mifuko ya Afya nchini Zambia.

Comments