BALOZI SEIF NA UFUNGUZI WA MAFUNZO YA WAKUFUNZI WA SENSA


Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar        

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Idd amesema mafanikio ya Sensa ya mwaka 2012 yanategemea umakini wa Wakufunzi wa Sensa ambao wanajukumu la kuhakikisha kuwa mafunzo waliyoyapata yanawafikia Makarani wa Sensa ili kuiwezesha Sensa ya mwaka huu kuwa na mafanikio zaidi ya mwaka 2002.
Balozi Seif ameyasema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya Wakufunzi wa Sensa ngazi ya Mkoa yaliyofanyika leo ukumbi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu
Amesema Wakufunzi hao wanajukumu kubwa la kuhakikisha Sensa ya mwaka 2012 inafanikiwa kwani wao ndio ambao wataenda kuwaelimisha makarani wa Sensa yale ambayo yanahitajika na kufanyiwa kazi.
“Dhamana ya mafanikio ya Sensa hii ipo mikononi mwenu,hivyo ni imani ya Serikali kuwa mtatumia juhudi na maarifa ili lengo hilo liweze kufanikiwa na kujenga imani kwa wananchi kwamba rasilimali zilizotumika zimeleta mafanikio yaliyokusudiwa” Amesema Balozi
Amefahamisha kuwa mafanikio ya Sensa yaliyopatikana mwaka 2002 yaliipa heshima kubwa Zanzibar katika nyanja za kimataifa na kupelekea baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Ghana, Angola,Sudani kuja kujifunza jinsi Zanzibar ilivyofanya sensa hiyo kwa mafanikio makubwa.
Ameongeza kuwa kutokana na matayarisho ambayo yamefanywa na Serikali ya Mapinduzi kwa kushirikiana na Serikali ya Muungano anaamin kuwa Sensa ya mwaka huu itakuwa na mafanikio zaidi ili iwe dira kwa nchi nyingine zaidi duniani.
Aidha amewataka Wakufunzi hao kuwatanabahisha makarani wa Sensa juu ya changamoto ambazo wanaweza kukabiliana nazo na njia za kuziepuka wakati wa zoezi la Sensa litakapoanza.

Comments